Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe na wenzake watatu, akiwamo Kepteni William Silaa wamefariki dunia katika ajali ya helikopta, ambazo wataalamu wanasema husababishwa na kosa la kibinadamu la rubani.
Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah alisema jana kuwa walipata taarifa ya ajali hiyo na kuthibitisha kuwa watu wote wanne waliokuwa kwenye helikopta hiyo walifariki dunia.
Miili ya Marehemu Filikunjombe, Kepteni Silaa na wengine iliwasili jijini Dar es Salaam jana jioni kwa helikopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu taratibu za mazishi.
Hii ni ajali ya sita ya ndege aina ya helikopta, maarufu kwa jina la chopa, katika kipindi cha miaka miwili huku Filikunjombe, ambaye alikuwa mbunge wa Ludewa kuanzia mwaka 2010, akiwa mgombea wa tano kupoteza maisha tangu mchakato wa Uchaguzi Mkuu uanze.
Mbali na ajali iliyomuhusisha Joshua Nasari mkoani Arusha, nyingine ilitokea Aprili mwaka jana ikimuhusisha mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal na kamanda wa Kanda Maalumu ya ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Chopa nyingine ilianguka Februari mwaka jana mkoani Mwanza ikiwa imebeba wanajeshi ambao wote walifariki na nyingine ilianguka Kipunguni Novemba, 2014 ikiwa imebeba marubani watatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambao pia walifariki.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema waliiona chopa hiyo ikiwa umbali wa kilomita nne na baadaye wakaona imeshika moto kabla ya kusikia kishindo kikubwa.
Sababu za ajali za chopa
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuelezea chanzo cha ajali iliyochukua maisha ya Filikunjombe na wenzake, lakini Mwananchi iliongea na mtaalamu wa mambo ya ajali za anga kutaka kujua sababu za ajali za chopa.
“Hakuna chopa inayoanguka kwa sababu ya ubovu wake,” anasema mtaalamu wa ajali za ndege, John Nyamwiura alipoulizwa na Mwananchi kuhusu chanzo cha ajali za chopa.
“Mara nyingi ajali hizo husababishwa na makosa ya rubani. Ubora wa chopa haujawahi kuwa chanzo cha ajali, chanzo kikubwa ni makosa ya rubani yanayochagizwa na hali ya hewa.”
Silaa, baba wa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jiji la Dar es Salaam, Jerry Silaa, ndiye aliyekuwa rubani wa helikopta hiyo iliyoondoka jijini hapa jana jioni kuelekea Ludewa mkoani Iringa.
Hiyo ni ajali ya pili kwa rubani huyo wa kampuni ya General Aviation Services baada ya kunusurika katika ajali nyingine ya chopa iliyotokea mkoani Arusha, akiwa amemchukua mbunge wa Arumeru Mashariki, Nasari na watu wengine.
Katika ajali ya Arusha, rubani huyo alifanikiwa kuipeleka chopa hiyo hadi juu ya mti ambako ilinasa na hivyo kuokoa maisha ya wote waliokuwa kwenye chombo hicho.
Filikunjombe, ambaye alijipatia umaarufu wakati wa sakata la Akaunti ya Escrow mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa makamu mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alipata umaarufu kutokana na msimamo wake wa kutaka wahusika wote kwenye kashfa hiyo iliyohusisha uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni, wachukuliwe hatua, akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa wa kwanza kuthibitisha kutokea kwa ajali hiyo, alisema mapema jana kuwa chopa hiyo iliangukia sehemu ambayo si rahisi kuifikia na kuahidi kutoa taarifa zaidi baada ya watu waliotumwa eneo hilo kufika.
Viongozi wamlilia Filikunjombe
Taarifa za kifo chake zilienea kwa kasi kuanzia juzi usiku na baada ya kuthibitika, viongozi mbalimbali walianza kutuma salamu za rambirambi wakieleza kuwa Taifa limepoteza mtu muhimu.
“Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya Filikunjombe na Silaa ambavyo nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helikopta,” alisema Dk Magufuli katika taarifa yake.
“Filikunjombe alikuwa mbunge mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mitano ndani ya bunge letu. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.”
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa alisema kifo cha Filikunjombe ni cha kushtua kwa kuwa alikuwa mwanasiasa chipukizi na jasiri.
“Ni pigo jingine kubwa ambalo katika kipindi kifupi Taifa limepata, huku bado likiwa na kidonda cha kuondokewa na wana siasa wengine mahiri, marehemu (Celina) Kombani, Dk (Abdallah) Kigoda na Dk (Emmanuel) Makaidi aliyefariki jana (juzi).”
Msemaji wa kampeni za CCM, January Makamba alisema Filikunjombe ameondoka mapema.
“Tunaambiwa tusihoji matakwa ya Mungu, lakini kuna nyakati inakuwa ngumu. Pole pia kwa Ndugu Jerry Silaa kwa kuondokewa na baba mzazi.”
Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa PAC pamoja na Filikunjombe alikuwa na masikitiko baada ya mbunge huyo wa Ludewa kufariki dunia.
“Nimepoteza rafiki. Nimepoteza ndugu. Nimepoteza mtu mtiifu kabisa kuwahi kuwa naye. Sina ya kueleza. Mungu ana mipango yake,” alisema Zitto Kabwe.
Mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema: “Ni masikitiko, ni pigo, ni pengo lisiloweza kuzibika. Deo Filikunjombe ametutoka, Taifa linahuzunika.”
Filikunjombe anakuwa mgombea ubunge wa sita kupoteza maisha tangu kampeni zianze Agosti 22. Mgombea wa Jimbo la Lushoto kwa tiketi ya Chadema, Fredy Mtoi alikuwa wa kwanza kupoteza maisha baada ya kampeni kuanza.
Baadaye Kombani, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), alifariki akiwa nchini India ambako alikuwa akitibiwa. Alikuwa anatetea ubunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki.
Kifo chake kilifuatiwa na mgombea wa Jimbo la Arusha Mjini, Estomih Mallah aliyefariki akiwa KCMC mkoani Kilimanjaro alikokuwa akitibiwa shinikizo la damu, na kufuatiwa na kifo cha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda ambaye alikuwa mgombea wa Jimbo la Handeni. Dk Makaidi alikuwa akigombea ubunge Jimbo la Masasi.
Pia mwanasiasa maarufu nchini, Mchungaji Christopher Mtikila alifariki kwa ajali ya gari wiki mbili zilizopita.
Miili yawasili, imeharibika vibaya
Mwili wa Filikunjombe na wenzake iliwasili jana saa 10:30 jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na kupokelewa na viongozi mbalimbali, akiwamo Spika Anne Makinda, Kashililah na baadhi ya wabunge.
Baada ya kupokewa, askari waliipakia miili kwenye magari matatu tofauti na msafara wa magari 15 ulielekea Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ambako ilihifadhiwa kusubiri taratibu nyingine.
Zitto, ambaye ni msemaji wa familia, alisema kwa kuwa miili hiyo imeharibika sana na hivyo taratibu za mazishi hazitachukua muda mrefu.
“Itachukua siku moja au mbili, kwa sasa madaktari wanaifanyia uchunguzi kuitambua,” alisema.
Habari za ziada na Fidelis Butahe