MTETEZI wa kiti cha ubunge, jimbo la Kilwa Kusini, Suleiman Bungara
“Bwege” anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina hali mbaya katika jimbo
hilo na hakuna namna yoyote ya kukiokoa na anguko la mara ya pili katika
uchaguzi mkuu. Anaandika Charles William … (endelea).
Bungara aliyeingia kwa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
akimuangusha kada kigogo wa CCM, Ramadhan Madabida, anasema siri ya
mafanikio hayo ni maendeleo aliyowapatia wananchi jimboni.
Ameiambia MwanaHALISI Online kwamba “Huku Kilwa kusini kila kitu kimekaa
sawa, nimefanya kazi kwa miaka mitano na kila mtu ameshuhudia
nilivyokuwa nikipambana ndani na nje ya bunge kupigania maslahi ya watu
wa Kilwa na Lindi kiujumla.”
Amesema kwamba anachofanya sasa ni kukumbushia yale aliyoyafanya pamoja
na kueleza atakavyoshughulikia yaliyobakia katika kipindi cha miaka
mitano ijayo.
Bungara anayefahamika zaidi kwa jina la utani la Bwege, amesema tangu
ameanza kampeni zake, wananchi wanampokea vizuri kila anapofika kuomba
kura na wameonesha kuridhika na jitihada zake.
Bungara anakabiliana na ushindani wa Hasanain Gulamabas Dewji kutoka
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye Bwege anasema hamhofii kwa kuwa, “CCM
ipo taabani sana huku kwa sasa, wananchi wa Kilwa hawapo tayari kurudi
tena utumwani, walishaamka na hawataki kurudi katika usingizi mzito
utakaowachelewesha kufanya shughuli za maendeleo.”
Bwege anaungwa mkono na vyama vinne vikiwemo NCCR-Mageuzi na National
League for Democracy (NLD) ambavyo vimeshirikiana na Chadema na CUF
kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Anasema ameshafanya kampeni katika Kata zote 10 za jimbo na kuzunguka
vijiji vyote 38; sasa akiwa ameanza duru la pili la kuzunguka ili
kuongeza morali wa umma kumchagua tena.