TAMKO RASMI LA BALOZI JUMA V. MWAPACHU.
NAJIVUA UANACHAMA WA CCM
Ndugu zangu,
Kesho ni siku muhimu katika kalenda ya
Taifa letu. Tunamkumbuka marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliyetutoka miaka 16 iliyopita. Nadhani ni siku
mwafaka kwangu kufanya maamuzi magumu katika maisha yangu ambayo
yanahusu uanasiasa wangu. Mimi ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 1967
wakati nilipojiunga na TANU Youth League. Nimepata fursa ya kuwa
kiongozi ndani ya Chama hiki. Lakini kuanzia kesho mimi si mwanachama wa
CCM tena. Natoa maelezo yafuatayo:
Kwa kipindi chapata mwezi na nusu hivi
sasa mmekuwa mkisoma makala zangu kuhusu msimamo na mwelekeo wangu
katika masuala ya siasa za hapa nchini hususan kuhusu uchaguzi mkuu na
mstakabali wa demokrasia nchini mwetu. Nyote mnatambua kwamba kuanzia
mchakato wa kumpata mgombe wa Urais ndani ya CCM kule Dodoma, ambako
nilipiga kambi, sijayumba katika msimamo wangu kwamba Edward Ngoyai
Lowassa ndiye chaguo langu katika kampeni za kumpata Rais mpya wa Taifa
letu.
Chaguo langu si ndoto wala mlipuko wa
mapenzi juu ya Lowassa. Nimemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 nikiwa
cadre wa Chama cha Mapinduzi kwa mahusisho katika majukumu ya Kichama.
Lowassa amejaaliwa nuru na uwezo wa kuongoza na wa kupendwa na watu. Ni
msikivu pamoja na kwamba ni kiongozi asiyependa ukiritimba na utovu wa
nidhamu, iwe kwa upande wa watumishi au wananchi wenyewe. Kubwa kwake ni
ucha Mungu wake ambao unamsaidia sana katika uongozi unaojali na
kuheshimu utu, ukweli na uwazi. Wanaodhani au kutaharuki kwamba eti
anaweza au ana hulka ya kulipiza kisasi kwa jambo lolote lile ni waongo;
wanajilinda.
Lowassa ni chaguo la wengi na CCM,
katika busara yake ya kumuengua katika mchakato wa kumpata mgombea wa
Urais, kimedhihirisha kutokuwa Chama kinachoendeshwa kwa misingi ya
demokrasia. Dalili za Chama hiki kupoteza lengo la kuwa Chama cha watu,
na kuwa cha viongozi wachache zilianza siku nyingi na hasa katika
kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. CCM
kimebadilika na kuwa Chama cha makundi na migawanyiko yakupambana, si
kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa Chama, bali ya kumalizana na kutaka
kufukuzana.
Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi
tu iliyopita! Aliweza kushinda vita hivyo kutokana na kupendwa na wengi
ndani ya CCM. Hivyo, kujitoa kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni
sahihi kabisa kwasababu CCM si Chama tena cha watu. Kimetekwa. Na mimi
nakubaliana na msimamo wa Lowassa na hao waliyofuata kutoka nadani ya
CCM.
Niliwahi kuandika makala katika ukurasa
huu nikimnukuu mshairi mmoja wa Uingereza aliyeandika kwamba, ‘there
comes a time when the door opens and allows the future in’. Mlango huo
sasa umefunguka usoni mwangu na huu uamuzi wangu maana yake ni kukubali
kwamba wakati mpya umewadia; ni wakati wa mabadiliko. Kuendelea kujihisi
kwamba ningali mwana CCM wa kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe. Si
sawa. Kama marehemu Baba wa Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama
yangu’.
Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho mimi si
mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya
kata yangu Mikocheni, Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na Chama
kingine.
Mwenyezi Mungu anilinde.