Dar es Salaam. Mikoa tisa ndiyo itakayoamua mshindi wa kinyang`anyiro cha urais, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.
Mgombea
aliyechanga karata zake vyema kwenye mikoa hiyo, atakuwa na uwezo wa
kuvuna takriban kura milioni 12 ambazo haziwezi kupatikana kwenye mikoa
mingine 21 iliyosalia, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mapema wiki hii, NEC
ilitangaza idadi ya mwisho ya wapigakura waliojiandikisha kuwa ni
milioni 22.75 watakaogawanywa katika vituo 65,105, kila kimoja kikiwa
kimepangiwa wapigakura wasiozidi 450.
Kutokana na
mgawanyo wa wagipakura hao kwa mikoa yote 30 nchini, Mwananchi
limekokotoa na kubaini kuwa mikoa tisa yenye idadi kubwa ya wapigakura
inaweza ikaamua mshindi kutokana na kila mmoja kuwa na zaidi ya
wapigakura milioni moja.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Tabora, Dodoma, Kagera, Tanga na Arusha.
Mgombea
urais wa CCM, Dk John Magufuli na wa Chadema, Edward Lowassa wamekuwa
wakizungukia mikoa mitatu kati ya hiyo - Dar es Salaam, Arusha na Mbeya -
kwa nyakati tofauti, wakiingia na kutoka isipokuwa Mwanza pekee ambako
wote wawili walisita kuingia wakisubiri ngwe ya mwisho.
Mkoa
unaoongoza kwa idadi kubwa ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura ni
Dar es Salaam wenye wapigakura 2,775,295 ukifuatiwa na Mwanza
(1,448,884), Mbeya (1,397,653) na Morogoro (1,271,951).
Idadi
ya wapiga kura kwenye mikoa mingine ni Tabora (1,097,760), Dodoma
(1,071,383), Kagera (1,051,681), Tanga (1,009,753) na Arusha
(1,009,292). Mikoa hii pekee inatoa ushindi wa zaidi ya asilimia 53
ambao unatosha kumpeleka mgombea husika Ikulu.
Dar es
Salaam yenye zaidi ya asilimia 10 ya wapigakura wote imevutia macho ya
vyama vyote vikubwa ambavyo licha ya kuzindulia kampeni zake, pengine
vitalazimika kufungia kampeni zao za uchaguzi pia.
Umuhimu
wa Dar es Salaam ni kwamba yeyote atakayepata kura nyingi, hata akikosa
katika mikoa minane iliyobaki, anaweza akashinda akifanya vizuri kwenye
mikoa 21 iliyobaki ambayo ina takribani wapigakura milioni 10.
Ukiacha
mikoa yote ya Zanzibar, mikoa minane yenye idadi ndogo zaidi ya
wapigakura ambayo ni sawa na asilimia 18.6 tu kwenye ushindi wa rais, ni
pamoja na Katavi (322,127), Njombe (383,366), Rukwa (459,573), Lindi
(514,558), Iringa (529,887), Singida (648,897), Manyara (678,586) na
Pwani (697,533).
Mikoa mingine yenye kura nyingi ambazo
pia zinachangia kwa kiwango kikubwa kwenye ushindi kwa asilimia 28.4 ni
Mara (892,741), Geita (887,982), Kilimanjaro (800,349), Kigoma
(792,551), Shinyanga (773,273), Ruvuma (739,774), Mtwara (728,981) na
Simiyu (718,777).
Wapigakura wote 503,193 wa Zanzibar
watalazimika kupiga kura mara tano ikiwa ni kura za rais wa Serikali ya
Mapinduzi (SMZ), mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, sheha, mbunge na rais
wa Muungano. Kati ya hao 48,182 watafanya hivyo kwa rais wa Muungano na
mbunge pekee.
Mkurugenzi wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa NEC, Dk
Modestus Kipilimba alisema uhalali wa wapigakura wa Zanzibar unatokana
na taratibu zilizopo visiwani humo.
"Kuna sheria ya
uchaguzi inayomtambua anayeruhusiwa kuchagua mbunge na Rais wa Muungano
huku ikimzuia kufanya hivyo kwa viongozi wa visiwani pekee. Yule
anayechagua viongozi wa Zanzibar anaruhusiwa kwa wote, hivyo hao 48,000
wamebanwa na vigezo vilivyowekwa," alisema.