Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na ya Japan, zimetiliana saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (flyover) na Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction utakaogharimu zaidi ya Sh87 bilioni.
Ujenzi huo ambao utafanyika katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, eneo la Tazara jijini Dar es Salaam utaanza mwezi huu na ukamilika katika kipindi cha miezi 35.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, alisema Serikali imekuwa ikihangaika kwa zaidi ya miaka saba ili kupunguza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam.
"Nawashangaa wanasiasa wengine wanapanda majukwani na kusema wataondoa tatizo la foleni kwa siku 90 wakati kupata mkandarasi tu imechukua miaka mingi. Ujenzi wenyewe hadi kukamilika ni zaidi ya miaka miwili,"alisema.
Dk Magufuli aliishukuru Serikali ya Japan kwa kukubali kujenga barabara hiyo ya juu kwa bei inayoendana na bajeti iliyotengwa na kuitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuusimamia vema mradi huo.
Awali, akizungumzia sababu za kuchelewa kwa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema ilitokana na kupandishiwa bei na makandarasi waliokuwa wakipewa kazi hiyo.
"Utiaji saini wa mkataba wa mradi huu ni faraja kwa wakazi wa jiji hili, kwani ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu ili kupunguza kero ya msongamano wa magari,"alisema.