Mikoa
ya Rukwa, Katavi, Iringa, Mbeya na Njombe imekuwa kimbilio la Taifa
wakati wa njaa, lakini wanasiasa wana sababu nyingine ya kuwahishia
kampeni zao Nyanda za Juu Kusini ambako kuna kura takriban milioni 3.92.
Eneo
hilo linajumuisha mikoa inayojulikana kama The Big Four, yaani Mbeya,
Iringa Ruvuma na Rukwa, ambayo ni maarufu kwa kuzalisha chakula, lakini
wagombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wanaliangalia eneo hilo
kwa jicho tofauti; linaweza kuamua mshindi wa mbio za urais.
Dk
John Magufuli, mgombea urais wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema
walizindulia kampeni zao jijini Dar es Salaam, lakini mara baada ya
kuzindua tu walichomoka kuelekea mikoa hiyo.
Kwa
mujibu wa Makadirio ya Idadi ya Wapigakura 2015 yaliyofanywa na Taasisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mkoa wa Mbeya ulikadiriwa kuwa na wapigakura
1,477,370, Rukwa (472,790), Iringa (524,390), Katavi (271,160), Ruvuma
(783,296) na Njombe (392,634).
Dk
Magufuli, ambaye ndiye aliyefungua pazia la kampeni Agosti 23 kwenye
viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam, alihamia Mkoa wa Katavi na
baadaye Mbeya na Iringa, wakati Lowassa, ambaye alikuwa wa pili kufanya
uzinduzi jijini Dar es Salaam, alichomokea mkoani Iringa na baadaye
kwenda Njombe, Ruvuma na Rukwa.
Chama
cha ACT-Wazalendo pia kilizindulia kampeni zake Mbagala, na awali
kilipanga kufanya harakati zake mikoani kwa kuanzia Mkoa wa Morogoro,
lakini jana chama hicho kilitangaza kuwa kinaelekeza nguvu kwanza Mkoa
wa Katavi.
January Makamba
“Ni
ratiba tu. Sisi tunafuata ilivyopangwa,” alisema January Makamba, mmoja
wa makada wawili walioteuliwa na CCM kuwa wasemaji wa shughuli za
kampeni za uchaguzi za chama hicho.
Makamba
alisema kitendo cha chama hicho tawala kuanzia kampeni zake mikoa ya
Nyanda za Juu Kusini, hakimaanishi kwamba kinabagua baadhi ya maeneo,
bali ni utaratibu waliojiwekea.
“Maeneo
yote ya Tanzania ni sawa na tutahakikisha tunafanya kampeni zetu kila
sehemu ya nchi hii na ndiyo maana tunatumia barabara wala siyo usafiri
wa anga,” alisema Makamba.
“Kwa
kuwa sisi tulikuwa wa kwanza kufungua pazia la kampeni na kuanzia huko,
basi na wenzetu wakaamua kutufuata kule tulipoanzia.”
Chadema watetea
Ofisa
habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama hicho kilianza kampeni
zake ukanda huo kutokana na mikakati ambayo chama iliweka kwa muda
mrefu.
“Chama chetu kimegawanya kanda 10, ni uamuzi wa chama kupanga kianzie wapi mashambulizi ya kisiasa,”alisema Makene.
Aliongeza: “Hiyo ni sababu moja lakini sababu kuu iliyotufanya tuanzie kampeni huko, hiyo ni siri ya chama.”
Alizitaja kanda hizo kuwa ni Nyasa, Victoria, Serengeti, Kusini, Magharibi, Kati, Pemba, Unguja, Kaskazini na Pwani.
Pamoja
na maelezo hayo, mikoa hiyo, ambayo hadi sasa ina jumla ya wabunge
wanne kutoka vyama vya upinzani, imeonekana kuendelea kuwa na mwamko
mkubwa wa kisiasa katika miaka ya karibuni.
Katika
uchaguzi wa mwaka 2010, vyama vya upinzani vilifanikiwa kuingiza
wabunge wanne tu kutoka mikoa yote ya kanda hiyo, lakini kumekuwa na
ongezeko kubwa la mwamko wa wananchi kisiasa uliosababisha vyama hivyo
kushinda viti vingi vya serikali za mitaa na vijiji.
Kwa
mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba
2014, CCM ilishinda mitaa na vijiji 9,406, wakati vyama vya upinzani
viligawana nafasi 3,211, hilo likiwa ni ongezeko la viti 1,981
ikilinganishwa na uchaguzi wa 2009.
Mkoani
Mbeya pekee, vyama vya upinzani vilishinda zaidi ya mitaa, vitongoji na
vijiji 600, ikiwa ni ongezeko kubwa kulinganisha na mwaka 2009.
Wachambuzi
wa masuala ya kisiasa waliohojiwa na Mwananchi kuhusu kitendo cha
wagombea hao kuipa kipaumbele mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wameeleza
kuwa inatokana na haja ya kuwahi kura kwenye eneo ambalo wanasiasa
wanadhani lina wapigakura wengi ambao wanaweza kubadilika baada ya
kuhamasishwa.
Dk Mwakajumulo
Dk
Steven Mwakajumulo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku),
alisema mazingira na hali ya kisiasa katika mikoa hiyo yamebadilika
kwani asilimia kubwa ya wananchi wake wanaonekana kutotabirika licha ya
baadhi yao kuhitaji mabadiliko ya uongozi wa serikali.
Alisema mwamko huo umesababisha CCM na Ukawa kuanzia maeneo hayo ili kutengeneza ushawishi wa mapema kwa wananchi hao.
“Idadi
kubwa ya wananchi wake wamekuwa na mwamko, na kwa sasa ni miaka mitano
tangu uchaguzi wa mwaka 2010, kwa hivyo kila mmoja anataka kuwahi
kumiliki wapigakura wa nyanda hiyo ya kusini,” anasema.
“Kikubwa
zaidi ni mwamko uliochangiwa zaidi na msingi wake wa kuwa chimbuko la
vyama vya wapigania uhuru. Kwa hivyo ni mbinu za kuwahi ngome hiyo. CCM
inataka kurejesha heshima yake ya zamani na Ukawa wanataka kuteka kundi
linalohitaji mabadiliko, ndiyo maana wameanzia huko.”
Wakati
Dk Mwakajumulo akizungumzia nia ya wanasiasa kuwahi kujenga ngome
kwenye eneo hilo, Profesa Gaudence Mpangala, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Ruaha mkoani Iringa, anaona sababu kubwa ni kukosekana kwa uimara wa
mgombea licha ya kuwepo upepo wa mabadiliko.
“Kwa
kuwa wagombea hao wana ngome zao zinazojulikana, wametumia nafasi hiyo
kuanza na maeneo magumu ili kutengeneza mazingira ya kujihakikishia
hesabu za wapiga kura katika maeneo hayo,” alisema.
“Ukawa
wana ngome yao (mikoa ya) kaskazini na CCM wanaonekana kuwa na ngome
yao Kanda ya Ziwa, kwa hivyo kuanzia maeneo magumu hayo inaweza kuwa
hesabu nzuri kisiasa.
“Mwaka
2010, CCM ilipoteza majimbo mengi na kukosa uaminifu kwa hivyo kabla ya
maeneo mengine, lazima wajipange vizuri maeneo hayo na zaidi ni kutaka
kuyarudisha mikoani mwao.”
Naye
Emmanuel Mallya, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Idara
ya Sayansi ya Siasa, alisema kuna siri kubwa iliyopo kwa wagombea hao
kuanzia kampeni zao mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, lakini kuanza kwa
kasi katika kampeni ni humu zaidi ili kutengeneza ushawishi katika
mwendelezo wa mikoa mingine.
“Ninachoamini,
katika kuanza lazima ujenge ushawishi kwa kupata mwitikio mkubwa.
Inawezekana CCM na Ukawa kimahesabu wameona kule ndiyo sahihi,” alisema
Mallya.
“Pia kwa sasa Nyanda hiyo itakuwa na idadi kubwa ya kura kwa hivyo lazima wapiganie kwanza maeneo hayo,” alisema Mallya.