Nyumba za Mawaziri zilizojengwa katika eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam. Serikali imewataka Mawaziri hao kuhama baada ya kipindi chao cha uongozi kumalizika
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri
kufahamu sura zitakazoingia kwenye baraza jipya la mawaziri katika
Serikali ya Rais John Magufuli, baadhi ya mawaziri wa awamu iliyopita ya
Jakaya Kikwete hawajaziachia nyumba za Serikali walizokuwa wanaishi.
Kwa
mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma, mawaziri wanastahili kuishi
kwenye nyumba za Serikali kuanzia pale uteuzi wao unapotangazwa ili
kuanza kutekeleza majukumu yao wakiwa katika mazingira salama, wao na
familia zao. Haki hiyo hukoma mara moja; pale wanapovuliwa wadhifa huo
au baraza husika linapovunjwa baada ya kukamilisha muhula wake au sababu
nyingine yoyote.
Maandalizi ya Rais Magufuli katika
uteuzi yanakwenda sambamba na taasisi zinazohusika kutekeleza wajibu wao
wa kuandaa makazi ya wateule wanaotarajiwa, lakini zinakwamishwa na
mawaziri ambao hawajahama.
“Tumepata fedha za kutosha
kukarabati nyumba zenye uhitaji huo kutoka wizarani. Nyumba 15 zipo
katika utekelezaji. Kuna baadhi tunasubiri waliomo wahame ili tuweze
kuendelea,†alisema Mhandisi Edwin Nnunduma, kaimu mkurugenzi wa
ushauri wa Wakala wa Nyumba za Serikali Tanzania (TBA).
Nnunduma
alisema kila kitu kipo tayari na mapokezi ya viongozi hao
hautacheleweshwa kwa namna yoyote ile kwa kuwa nyumba zipo za kutosha
kuwahifadhi ili walitumikie Taifa kwa viwango vinavyohitajika.
Takwimu
zinaonyesha kuwa wakala huyo anasimamia jumla ya nyumba 93 na kati ya
hizo 29 zilikuwa zinakaliwa na mawaziri wa Serikali iliyopita ya Rais
Jakaya Kikwete ambao, kwa mujibu wa kanuni walistahili kuziachia mara tu
baada ya Rais Magufuli kuapishwa, Novemba 5.
Kwa
mujibu wa Nnunduma, ukarabati huo unahusisha nyumba 35 ambazo
zinajumuisha 29 za mawaziri na sita wanazoishi baadhi ya makatibu wakuu
wa wizara.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi zinaeleza
kuwa wapo baadhi ya mawaziri ambao wamekaidi kuondoka kwenye nyumba
hizo, licha ya kanuni na sheria kuwataka kufanya hivyo na agizo la
Katibu Mkuu Kiongozi lilikwishatolewa likiwataka kurudisha magari na
nyumba za Serikali.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo,
Mnunduma alisema, “Kuna waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi uliowataka
wahame kwenye nyumba hizo ndani ya siku 30 baada ya kuapishwa kwa Rais
mpya. Muda huo uliisha jana (juzi), naamini bado baadhi hawajahama mpaka
sasa. Nilikuwa safarini hivyo sina uhakika ni nani na nani hawajafanya
hivyo.â€
Novemba 5, mara baada ya kuapishwa kwa Rais
Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, aliwaagiza mawaziri na
manaibu waziri kurudisha magari ya Serikali ikiwa ni siku yao ya ukomo
wa uongozi. Katika agizo hilo, alisema baada ya bendera ya Rais
anayemaliza muda wake kuteremshwa na kabla ya ile ya Rais mpya
kupandishwa, magari hayo yanatakiwa yabadilishwe namba kwa kuondoa
herufi ya cheo na kuwekwa zile za Serikali.
Wakati
urejeshaji wa magari ulifanywa mara moja, uhamaji kwenye nyumba za
Serikali ulipewa muda wa siku hizo 30, ili kutoa fursa kwa familia
husika kuandaa mazingira hayo ikiwa ni pamoja na kusafirisha mali husika
za viongozi hao na walio nao.
Kukawia huko kwa baadhi
ya mawaziri kunaelezwa kuwa huenda kukawa na sababu mbili; ama uhakika
wa kurudi kwenye baraza jipya au kutokana na ukosefu wa mahali pa
kuhamia baada ya utumishi kukamilika na muda wa kutafuta mahali pengine
penye hadhi sawa na yao kuwa changamoto.
“Wapo baadhi
ya mawaziri ambao walichaguliwa siku za mwisho ambao kabla ya hapo
walikuwa wanaishi majimboni kwao. Mwezi mmoja uliotolewa unaweza
usitoshe kwa wao kutafuta nyumba nyingine hapa mjini itakayowafaa
kulingana na mahitaji yao,†kilisema chanzo ambacho hakikutaka
kutajwa.
Uchunguzi wa gazeti hili katika mitaa
Mikocheni, Masaki na Kijitonyama ziliko nyumba za mawaziri ulibaini
baadhi zikifanyiwa ukarabati na baadhi ya walinzi waliohojiwa
wakibainisha kuwa mawaziri wengi walishaondoka katika makazi hayo.
Hata
hivyo, ofisa wa TBA anayeshughulikia makazi ya mawaziri Kanda ya
Masaki, Juma Hamis alisema mawaziri waliokuwa wamebakia kwenye eneo lake
ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Hawa Ghasia.
“Kwa
taarifa nilizonazo, hawa mawaziri wanahama leo (jana) kwani tayari
wameanza kuhamisha baadhi ya vitu vyao,†alisema Juma.
Hata
hivyo, Makamba alipoulizwa alisema hajawahi kuishi kwenye nyumba ya
Serikali tangu aanze kuwatumikia wananchi kwa nafasi tofauti alizowahi
kuzitumikia.
Alisema, “Siku zote naishi kwenye nyumba yangu. Tangu nilipokuwa ikulu na hata nilipoondoka na kuwa waziri.â€