Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa amesifia kasi ya rais John Magufuli hasa katika kupambana na ufisadi nchini.
Dk. Slaa amesema kuwa alichowahi kukizungumzia awali kimetimia kwa kuwa nchi hii ilihitaji mtu kama Magufuli.
“Nadhani sasa unaelewa niliposhikilia msimamo wangu. Katika mazingira ya sasa Magufuli ni bora zaidi. Niliwahi kusema kuwa hii nchi kwa siku za mwanzo inahitaji udikteta kuirudisha kwenye mstari ulioonyooka, nimefurahi sana,” Dk. Slaa ameliabia gazeti la Raia Mwema.
Amesema kuwa Bunge linatakiwa kufanya kazi ya kuudhibiti udikteta huo ili usivuke mipaka lakini limuunge mkono kwa hatua anazochukua.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amemshauri Rais Magufuli kuiangalia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuifumua.
“Pasipo kuchukua hatua ya kuifumua Takukuru, sina hakika kama matarajio yatafikiwa,” alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa haraka.