Kwa niaba ya Rais Obama na watu wa Marekani, nawapongeza watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uchaguzi wa rais na wabunge ulioendelea kuthibitisha rekodi nzuri ya Tanzania katika kujenga demokrasia imara.
Wakati Rais John Pombe Magufuli na serikali yake wakichukua majukumu yao, tunatarajia kuendelea na ubia wetu wa karibu na kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya nchi zetu mbili tunapofanya kazi pamoja ya kusaidia ujenzi wa demokrasia, kukuza usalama wa kikanda na kuendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, napenda kumshukuru Rais aliyemaliza muda wake Jakaya Kikwete kwa jitihada zake za kujenga uhusiano imara na wa kudumu kati ya Marekani na Tanzania.
Hata hivyo, Marekani inaendelea kustushwa sana na tamko la mamlaka visiwani Zanzibar la kusudio la kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar wa Oktoba 25.
Kwa dhati kabisa, tunatoa wito kwa serikali mpya kuhakikisha kuwa maamuzi ya watu wa Zanzibar yanajidhihirisha katika ukamilishwaji wa haraka, wa haki na wa amani wa mchakato wa uchaguzi visiwani Zanzibar.