Mke wa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa,
Mama Regina Lowassa ambaye alishiriki kwa kiasi kikubwa katika
kukiongezea kura chama hicho na kuwapatia wabunge wengi kwa kuwashawishi
wanawake hivi karibuni alitangaza kuikataa zawadi ya Ubunge wa viti
maalum aliyepewa kwa heshima na chama chake hicho.
Ingawa Regina alikuwa mwanaharakati mkubwa wa kisiasa, alikataa
kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ambayo
wanasiasa wengi hutumia nguvu kubwa kuingia.
Kwa mujibu wa msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo, Regina Lowassa
alichagua kuendelea kuwatumikia akina mama nje ya Bunge kwa kuwa
anaamini atafanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi akiwa nje ya Bunge ambalo
lingemuongezea majukumu mengi.
"Ninawashukuru Kamati Kuu ya chama changu kwa heshima hii kubwa
waliyonipa na poia naithamini sana, lakini naamini nitaendeleza
mapambano ya kuwaletea mabadiliko akina mama kwa ufanisi zaidi nikiwa
nje ya Bunge," Liongo alimnukuu mama Regina Lowassa.
Kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Mama Regina Lowassa wakati wa
Kampeni, imedhihirisha wazi kuwa alikuwa na sifa za kuwa mbunge.
Chadema wamejipatia viti maalum 36 katika Bunge la 11 linalotarajia
kuanza rasmi Novemba 17 mwaka huu. Vyama vya Upinzani kwa ujumla
vimepata nafasi ya kuwa na wabunge 116 katika Bunge la 11, idadi ambayo
ni kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa vyama vya vingi nchini.