Na Mwandishi Wetu
MTABIRI maarufu nchini, Maalim Hassan
Yahya Hussein, amesema utabiri wake alioutoa mwaka 2014 kwamba mgombea
urais mmoja atafariki dunia ghafla kabla ya uchaguzi, umetimia baada ya
kifo cha Mchungaji Christopher Mtikila na kuwaacha salama wagombea
Edward Lowassa na Dk. John Magufuli.
Maalim Hassan aliyasema hayo
alipozungumza na gazeti hili juzi ambapo alisisitiza kuwa utabiri wake
alioutoa Desemba 28, 2014 katika mkutano wake na waandishi wa habari
ofisini kwake, haukumlenga mtu.
Mchungaji Mtikila ambaye alikuwa
akigombea urais kupitia Democratic Party (DP) kabla ya kuenguliwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alifariki dunia Oktoba 4, 2015 kwa
ajali ya gari kijijini Msolwa, Chalinze, mkoani Pwani akitokea Njombe.
“Nilipoutoa utabiri ule mengi yalisema
na watu wakawataja wagombea fulani, lakini niliwaambia kwamba utabiri
haulengi mtu na sasa umempata Mchungaji Mtikila.
“Mtikila alikuwa mgombea urais,
alichukua fomu na watu wakaona akiwa na mkoba kama wa wagombea wenzake,
akakataliwa na tume lakini akakata rufaa… angeweza pia kushinda rufaa
yake,” alisema Maalim Hassan.
Aliongeza kuwa, mara baada ya utabiri
wake alipigiwa simu na makada wa vyama viwili – Chama cha Mapinduzi
(CCM) waliodai kuwa mgombea wao Dk. Magufuli haumhusu na wale wa Chadema
nao wakasema mgombea wao, Lowassa hawezi kuchuliwa hivyo – akawajibu
wote kwamba utabiri wake haumlengi mtu.
“Niwahakikishie wananchi kwamba, kinyota
wagombea wote wa urais waliobaki sasa wako salama na watashiriki
kuchagua viongozi Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Maalim Hassan.