Chadema imewataka wananchi kujumlisha
matokeo yote yatakayotolewa kwenye vituo vya uchaguzi na kuyasambaza
badala ya kusubiri kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Akizungumza
jana kwenye mkutano wa kampeni Jimbo la Kikwajuni mjini Unguja, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema “ Bara, John Mnyika aliwataka wananchi hao
kutoondoka kwenye vituo vya kupigia kura, bali wasubiri hatua 200 kutoka
vituo hivyo kupiga kura ili kulinda kura zao.
"Mjitokeze
kwa wingi kupiga kura na baada ya kupiga kura mrudi nyuma hatua 200
kulinda ushindi wenu. Nina uzoefu na hili kwa sababu lilitokea jimboni
kwangu mwaka 2010," alisema na kuwataka Wazanzibari wasikubali kuibiwa
kura zao.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti
wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee aliyeambatana na
Mnyika katika kampeni za kumuunga mkono Salum Mwalimu anayegombea
ubunge wa Jimbo hilo la Kikwajuni, aliwaeleza wananchi kuwa uchaguzi wa
mwaka huu ni wa muhimu kwa sababu wakikosea kuchagua itawagharimu miaka
mingine mitano.
Alisisitiza kuwa kama wanataka kuwa na
mamlaka kamili, basi wamchague Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif
Hamad ili washirikiane kuanza upya mchakato wa Katiba. Aliwataka pia
wamchague Mwalimu kuwa mbunge wao ili akaongeze nguvu katika mapambano
bungeni na kuitetea Zanzibar.
"Moja ya ajenda kuu za
Ukawa ni kuwa na Muungano wa serikali tatu, Zanzibar ikiwa ni mamlaka
kamili. Wachagueni viongozi hawa ili mpate watetezi wenu watakaowaletea
maendeleo," alisema Mdee.
Awali, akiomba kura kwa
wananchi, Mwalimu aliahidi kwamba akichaguliwa, atahakikisha anasimamia
kikamilifu masilahi ya jimbo lake na Zanzibar kwa ujumla.
Alisisitiza
kuwa anatambua matatizo ya jimbo hilo na kuahidi kujitoa katika
kuyatatua kwa sababu naye pia ni sehemu ya jamii hiyo. Aliwataka
wananchi kumpigia kura kwa wingi Oktoba 25, ili atimize ahadi zake.