Taarifa za mchezo huo zinasema kwamba bia hiyo inatengenezwa na kiwanda kimoja kilichopo jijini Mwanza ambacho kinamilikiwa na mmoja wa makada maarufu wa CCM jijini.
Kwa sababu ya kuhofia usalama kwa kufichua mchezo huo, jina la kiwanda na mtu anayedaiwa kuwa mmiliki wake, yanahifadhiwa kwa sasa.
Mwandishi wa habari hizi amefahamishwa kuwa Oktoba 24, siku ya mkesha wa uchaguzi mkuu ambayo Mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli atafunga kampeni zake uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, kiwanda hicho kimeagizwa kutengeneza bia mbaya yenye kiwango kikubwa cha kilevi.
Mtoa taarifa amesema bia hiyo itagawiwa kwa vijana wanaoingia katika mkutano huo, hasa wale watakaotambuliwa si makada wa CCM, ili wakinywa, washindwe kuamka mapema Jumapili kwenda kupiga kura.
Amesema siku hiyo bia zitakuwa zinatolewa bure baada ya kila mmoja kuonesha kitambulisho mlangoni.
Mtoa taarifa amesema viongozi wa CCM wanauhakika kwamba jijini Mwanza sehemu kubwa ya vijana hawataki chama hicho na wamekuwa wakisikika kuwa watakayempigia kura ni mgombea urais anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa ambaye ameteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Lowassa ambaye anaungwa mkono na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, alifanya mkutano mkubwa wa kampeni hapa Jumatatu na kupata mapokezi makubwa yasiyowahi kutokea kwa miaka mingi.
Taarifa za mchezo mchafu unaodaiwa ni wa CCM, zinasema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vilivyo eneo la Igoma vyenye uzalishaji mkubwa.
“Lengo ni kutaka kupunguza idadi ya vijana ambao wengi wanaunga mkono upinzani, wewe mwenyewe kama unavyofahamu vijana wengi wanamkubali Lowassa… lazima wapunguzwe,” alisema mtoa taarifa huyo.
Jitihada za kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa juu wa CCM Mkoa wa Mwanza akiwemo Katibu wa Mkoa, Miraji Mtaturu, hazikufanikiwa.
Inadaiwa chama hicho kimeanza kuingiwa na wasiwasi kutokana na idadi kubwa ya vijana walio wengi kujiandikisha katika daftari la mpigakura na wamekuwa wakitamba kuwa kura zao wanazitia kwa wagombea wa UKAWA.
Pia hali ya hofu kwa CCM imeongezeka baada umma mkubwa wa vijana na wazee kujitokeza Oktoba 12 kumpokea na kumsikiliza Lowassa.
Hata hivyo baadhi ya wanasiasa waliozungumza na Mwanahalisi online wamesema Watanzania watakaohudhuria mkutano huo wanapaswa kuwa makini wasije wakaingia kwenye mtego wa kurubuniwa si hivyo watakosa kupiga kura ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kuiondoa CCM madarakani.
“Huwezi kukataza mtu kwenda kwenye mkutano wa kampeni, cha msingi waende kama ulivyoniuliza kuhusu tuhuma za bia, wasichukuwe, badala yake wasikilize sera na hoja na kuondoka mkutano ukiisha,” amesema mwananchi mmoja.
CHANZO CHA HABARI NI gazeti la >>MwanahalisiOnline ingia hapa<<