Ripota wetu yupo kituo cha Kimara Stop Over jijini Dar es salaam ambapo hadi sasa wananchi hawajapiga kura hadi muda huu. Tangu saa 12 asubuhi watu wamekusanyika kituoni lakini hakuna hata mmoja aliyepiga kura. Zaidi ya masaa 13 sasa akina mama, vijana na wazee wanasubiri kupiga kura,
Sababu za Kuchelewa
Sababu iliyotolewa na maafisa wa Tume ya uchaguzi ambao wamefika muda mfupi uliopita ni kwamba vifaa vya kupigia kura vimeharibiwa na wasimamizi wa uchaguzi waliokua wamepangwa eneo hilo baada ya kutoridhika na posho waliyopewa.
Mmoja wa Maafisa wa Tume ambaye hajajitambulisha jina lake amesema wasimamizi wa uchaguzi katika kituo hiki walikabidhiwa vifaa jana lakini wakaviharibu na kutokomea pasipojulikana na bado wanatafutwa na Polisi.
Wananchi Wahoji
Wananchi waliokua eneo hilo wamehoji ukweli wa taarifa hiyo na kutaka kudhibitisha kama kweli vifaa hivyo vimeharibiwa wavione.
Wengine wamehoji ni msimazi gani wa uchaguzi mwenye ujasiri wa kuharibu vifaa vya Tume? Hata hivyo Tume haijataja majina ya wasimamizi hao wanaodaiwa kuharibu vifaa.
Pia watu wamehoji hata kama vifaa vimeharibiwa je Tume haina vifaa vya ziada ili watu wapige kura? Ikiwa uchaguzi mkuu huandaliwa miaka mitano kabla ya kufanyika iweje pakosekane vifaa vya ziada? Tume ya Uchaguzi iliagiza vyama vya siasa viandae mawakala wa ziada, iweje wao washindwe kuandaa vifaa vya ziada?
Na kama Tume haikuwa na vifaa vya ziada vya kuwezesha uchaguzi kufanyika leo kwanini wameruhusu wananchi kwenda kituoni?
Hatua zilizochukuliwa
1. Waangalizi wa Kimataifa wamefika na kujionea hali halisi wakiwemo waangalizi wa SADC,
2. Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wamefika na kuelezea sababu za tatizo lakini hawakueleza suluhisho,
3. Mbunge wa Kibamba Mhe.John Mnyika amefika na kutuliza wananchi akiwataka waendelee kusubiri,
4. Jeshi la Polisi limeongeza idadi ya Askari wenye silaha, na magari yenye maji ya kuwasha pamoja na mbwa.!
Athari
1. Baadhi ya watu wameanza kuondoka kituoni,
2. Baadhi ya watu wamekatishwa tamaa baada ya kusubiri muda mrefu kituoni leo na pengine wasipate tena muda wa kupiga kura,