Mgombea urais kupitia chama cha TLP
Macmillan Lyimo amesema anaunga mkono kauli ya mwenyekiti wake wa chama
Mh. Augustine Mrema ya ‘kumpigia debe’ mgombea wa chama cha mapinduzi
CCM, Dk John Magufuli, kwa madai kuwa hayo ni maamuzi yake binafsi.
Akizungumza na EATV, Lyimo amesema kuwa
kauli hiyo haijatolewa na mkutano wowote wa chama, bali ni maoni binafsi
kwa kuwa mwaka huu watanzania wanachagua mtu na siyo chama na kwamba
jambo alilofanya Mrema si jipya wa la ajabu.
“Hili jambo siyo la ajabu, hata
Marekani, Colin Powell alitangaza kumuunga mkono Obama licha ya kuwa
chama tofauti, Mrema amesema hivyo kwa kuwa anajua looser siyo yeye,
tumesimamisha wagombea ubunge nchi nzima, na yeye ni mmoja wapo, kwahiyo
hilo halinipi shida” Amesema Macmillan Lyimo
Kuhusu mahusiano kati yake na mwenyekiti
huyo, Lyimo amesema kuwa mahusiano ndani ya chama hicho ni mazuri na
hakuna ugomvi wowote.
“Tunaendelea kushirikiana kama kawaida, na hata kampeni zangu nilianzia kwake na nitafungia jimboni kwake” kauli ya Lyimo
Kuhusu nafasi yake ya ushindi, Lyimo amesisitiza kuwa yeye ndiye atakayeshinda urais mwaka huu, na kamwe Rais hatoki CCM
“Magufuli hawezi kushinda, nafasi kubwa
ya ushindi ninayo mimi, hata Magufuli anajua kuwa mimi napinga huo
mwenge kwenye picha yake, hiyo ni ishara ya uchawi, na uchawi wake
utashindwa mwaka huu”. Amesema mgombea huyo