Hofu ilitanda jana katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es Salaam,
baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mashine ya kusajili wapigakura kwa
mfumo wa elektroniki (BVR) inatumika kuandikisha wafanyakazi katika
kiwanda hicho.
Kutokana na hofu hiyo, baadhi ya maofisa wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na Mwanasheria wa chama hicho, John
Mallya, Polisi na Tume Taifa ya Uchaguzi (Nec), walifika kiwandani humo
na kufanya upekuzi ikiwamo kuondoka na baadhi ya vifaa vilivyokuwa
vinatumika.
Baada ya kukubaliana pande zote, vifaa hivyo ambavyo ni vya kuchukua
alama za mikono, macho, scanner na kompyuta mpakato, vilichukuliwa na
Polisi ili baadaye vikakabidhiwe Nec.
Polisi, Chadema na Tume, walielezwa na Meneja Mawasiliano wa kampuni
hiyo, Abubakari Mlawa, kuwa kampuni hiyo imeamua kuandikisha wafanyakazi
wake kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika viwanda saba
walivyonavyo na kushindwa kuwatambua wafanyakazi.
“Tunaendesha zoezi la kuweka ‘data base’ kwa ajili ya wafanyakazi wetu
wote kwa maana ya kupiga picha na kuandika taarifa zake zote; amezaliwa
wapi, amesoma wapi na ameanza kazi lini, wakati tunaendelea na zoezi
letu walikuja watu wakajitambulisha kuwa ni polisi wakawaweka chini ya
ulinzi watu wanaofanya zoezi hilo. Tulipowauliza ni kina nani, walisema
wanatoka Chadema na wamepewa taarifa kuwa tunatoa vitambulisho vya
kupigiakura,” alisema na kuongeza:
"Ili tujiridhishe, tuliamua kuwaita Nec na polisi kuthibitisha
wamechukua mashine kwenda kujiridhisha. Tunafanya zoezi hili wiki nzima
na tumeandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 na tuna zaidi ya wafanyakazi
900.”
Hata hivyo, wakati anahojiwa na Polisi na Chadema kama kifaa cha alama
za vidole wametoa wapi, Meneja huyo alisema walitoa zabuni kwa kampuni
ambayo hakuitaja na alipotakiwa kuitaja hakufanya hivyo.
Afisa wa ICT wa Nec, Amosi Madaha, akizungumza mara baada ya kufika na
kulinganisha mashine ya alama za vidole ya Nec na yao, alisema ni mapema
sana kueleza kama vifaa hivyo ni sehemu ya vifaa vya BVR hadi
watakapokwenda kuvichunguza zaidi.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Nec, Salvisius Mkwera,
alisema walipata taarifa kuna uandikishaji wa wapigakura unafanyika
ndani ya kiwanda hicho na walipofika walikuta baadhi ya vifaa ambavyo ni
ngumu kusema.
“Tulichokiona ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya Tume,
lakini hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au siyo, tulichokubaliana na
polisi ni kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi tujiridhishe na
vifaa tulivyonavyo,” alisema.
Alitaja kifaa kinachofanana na cha Nec kuwa ni `finger print machine,'
lakini wamechukua na vifaa vingine kama kompyuta mpakato na scanner.
Alisema pia wataingia kwenye data base ya kampuni hiyo ili kujiridhisha na taarifa zilizoingizwa.
Alisema pia wamechukua orodha ya wafanyakazi waliorodheshwa kwenye
karatasi ili kuangalia kwenye daftari la kudumu la wapigakura kama kuna
uwiano wowote.
“Tutatoa taarifa mapema na kwa wakati ili kuondoa wingu lililotanda kwa
sasa, tunataka pande zote zijiridhishe hivyo tutafanya kwa uwazi kueleza
kama hizi ni mashine zetu,” alisema.
Baadhi ya wafanyakazi ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema
wameshtushwa na uandikishaji huyo kwa kuwa unafanana na BVR hasa kwenye
uchukuaji wa alama na kuamua kutoa taarifa.
Mpekuzi blog