MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusu
utangazaji wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa vyombo vya utangazaji kwa
mujibu wa Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa
Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015. Kanuni hizi zipo kwa mujibu wa
Sheria kama ilivyotolewa na Gazeti la Serikali la Tarehe 26 Juni, 2015.
Kanuni hizi zinalenga kuweka utaratibu mzuri wa kutangaza shughuli za
kampeni na uchaguzi mkuu kuwa wa amani na utulivu.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania inapenda kuwakumbusha kuwa ni marufuku kwa
vituo vyote vya utangazaji kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu bila
kupata taarifa sahihi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa
utaratibu waliojiwekea.
Vilevile,
vituo vyote vya utangazaji vinapaswa kuzigatia Sheria na Kanuni za
Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya
Siasa), 2015.
Kanuni
za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya
Siasa), 2015, Na. 16 (1) na 16(2) inaelekeza kama ifuatavyo:-
16(1)
kwamba kila mtoa huduma za maudhui atakuwa na wajibu wa kuuarifu umma
juu ya matokeo ya uchaguzi, kadiri yanavyopatikana. uangalizi maalumu
ufanyike kuhakikisha usahihi wa matokeo yote yanayotangazwa.
16(2)
Mtoa huduma za maudhui hatatangaza maoni ambayo yanaweza kuchochea
vurugu au kuhamasisha chuki kwa misingi ya mbari, kabila, jinsia, dini
au Imani za kisiasa na ambayo yanajenga uchochezi wa kusababisha
madhara.
Hivyo
basi, vituo vya utangazaji vinatakiwa kufuata kikamilifu Kanuni za
Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya
Siasa), 2015 na kwamba vituo vya utangazaji vitawajibika na matokeo ya
maudhui ya matangazo ambayo hayatozingatia Kanuni.
Mamlaka
inatoa wito kwa vituo vya utangazaji kutumia weledi katika maamuzi ya
kihariri kuchanganua kipi kinafaa kutangazwa na uangalizi maalumu
ufanyike kuhakikisha kuna usahihi katika kutangaza matokeo yote
yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
IMETOLEWA NA:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAREHE 25/10/2015