TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI, DAR ES SALAAM, ALHAMISI, 17 SEPTEMBA 2015
USHIRIKI WA VYAMA VYA NCCR – MAGEUZI, NLD, CUF NA CHADEMA KATIKA UKAWA.
UTANGULIZI
Sisi viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu tukiwa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa na viongozi wengine, tumekuja mbele yenu mtusaidie kufikisha ujumbe maalum kwa wanachama wetu na Watanzania wote wanaokiamini chama chetu,
Tumefika kuelezea kutoridhishwa na mwenendo wa ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA. Tumekuja pia kuwaelezea ni hatua gani tulizoamua kuchukua kukabiliana na changamoto hii.
Wengi wenu mnafahamu kuwa UKAWA ni Umoja wa Katiba ya Wananchi ulionzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba kutetea Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi dhidi ya uchakachuaji uliokuwa unafanywa na CCM.
UKAWA siyo chama cha siasa bali umoja. NCCR-Mageuzi iliamua kujiunga na harakati hizi kwa nia njema ya kutetea maslahi ya taifa letu. Zaidi ya mwaka sasa tangu tujiunge na umoja huu, matokeo yake yamekuwa ni mabaya kwa uhai na ustawi wa chama chetu. Wakati vyama vingine vimezidi kuimarika ndani ya UKAWA, NCCR-Mageuzi imedhoofika. Hali hii haikubaliki.
MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO BAINA YA VYAMA VYA UKAWA
Vyama vinavyounda UKAWA, vilisaini Makubaliano ya Ushirikiano katika Mkutano wa Hadhara kwenye viwanja vya Jangwani. Kitendo hicho kiliwavutia na kuwapa matumaini wananchi na wao wakazidi kutuunga mkono. Iliamuliwa kwamba tusiuwe vyama vyetu bali tuunganishe nguvu za vyama vyetu kama namna ya kujiimarisha kwa pamoja.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA DISEMBA 2014.
Kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, vyama vinavyounda UKAWA vilitiliana saini ya Mwongozo wa Ushirikiano katika Uchaguzi huo.
Licha ya kutiliana saini Makubaliano hayo, bado kulikuwa na ukiukwaji mkubwa na wa makusudi wa Mwongozo huo.
Licha ya kuzijadili changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi huo, lakini hazikupatiwa ufumbuzi wowote.
Sisi tuliopo hapa tulionya mapema kuhusu mwenendo huu wa kuvunja makubaliano na tukaomba taratibu tulizokubaliana zitumike ili kurudi kwenye misingi ya UKAWA lakini hatukusikilizwa.
USHIRIKIANO KATIKA UCHAGUZI MKUU, OKTOBA 2015.
Licha ya changamoto zilizokuwepo, tuliamua kwa pamoja kwamba vyama vya UKAWA tuingie katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na makubaliano ya ushirikiano, ikiwemo kuwa na mgombea mmoja wa Urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi.
Pia, katika kuendesha umoja huu, tuliunda vyombo vya kutusaidia ambavyo ni:-
- Kamati ya Wenyeviti.
- Kamati ya Makatibu Wakuu.
- Kamati ya Ufundi.
- Kamati ya Wataalam.
Pamoja na kuunda vyombo vya kuendesha UKAWA, tangu Januari 2015, bado tumeshindwa kujenga UKAWA imara na tuliyotarajia kwa manufaa ya wanaukawa na wananchi kwa ujumla.
Yafuatayo yamethibitisha hili jambo:
- Tumeshindwa kuweka Kanuni za uendeshaji wa UKAWA kama tulivyokubaliana. Kwa maana hiyo,tunafanya mambo kiholela
- Tumeshindwa kuunda Kamati zitakazoshughulikia migogoro baina ya vyama.
- Tumeshindwa kuunda na kuzisimamia Kamati za Majimbo
- Tumeshindwa kupata muafaka wa kuachiana majimbo.
Mfano, NCCR – Mageuzi tuliachiwa majimbo 12 ya Kasulu Vijijini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini, Manyovu, Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe mjini. Ikumbukwe kwamba, mwaka 2010, NCCR-Mageuzi ilisimamisha wagombea katika majimbo 67.
Kwa maana hiyo, UKAWA umeturidisha nyuma katika kupata wabunge na kuimarisha chama zaidi ya miaka 20 baada ya kuundwa kwake.
Licha ya kukubaliana kwamba NCCR-Mageuzi iachiwe majimbo 12, wenzetu wa vyama vingine katika UKAWA wamesimamisha wagombea katika majimbo 6 kati ya hayo. Wametuvunja moyo na kutuonyesha kwamba hawatujali. Na hata kule ambapo katika majimbo sita ambapo wametuachia bado wenzetu wanatufanyia fujo kuliko hata wanazotufanyia wanachama wa CCM. Tunamifano mingi ya kuonyesha ni jinsi gani wagombea wetu wanavyofanyiwa vurugu.
- Tumeshindwa kupata muafaka wa namna ya kuachiana wagombea udiwani katika kata nyingi.
- Tumeshindwa kuonesha na kukubaliana kila chama kitapata nafasi gani na ngapi katika Serikali ya UKAWA.
- Tumeshindwa kufuata utaratibu wa kumpata mgombea Urais wa UKAWA
- Tumeshuhudia vurugu kubwa iliyoletwa ndani ya UKAWA na wanachama waliotoka CCM na wao kupewa umuhimu kuliko viongozi wa UKAWA. Zaidi ya Mbatia hakuna kiongozi wa NCCR-Mageuzi anayeshirikishwa, anayezungumza au aliyepo kwenye kampeni za mgombea Urais wa UKAWA.
- Tumeshindwa kuwa na timu ya kampeni timu ya UKAWA, ambayo inagharamiwa na UKAWA na inatafuta fedha pamoja, kama ilivyokubaliwa.
- Tunashuhudia UKAWA ambayo Chadema ndiyo UKAWA-Bara na CUF ndio UKAWA-Zanzibar. Chadema haijali Zanzibar na CUF haijali Bara. Na NCCR-Mageuzi haipo huku wala kule ikiendelea kudhoofika siku hadi siku.
- Tumeshindwa kuona uwazi katika matumizi ya fedha na maamuzi muhimu ya uendeshaji wa UKAWA.
- Tumefadhaishwa na kuvunjwa kwa misingi ya kuanzisha kwa UKAWA.
- Wakati NCCR imetii mgawanyo wa majimbo kwa vyama vinavyounda UKAWA, vyama vingine na hasa CHADEMA vimesimamisha wagombea kinyume cha makubaliano.
NINI KIFANYIKE NA UKAWA
Hatukuwaita hapa kuwaambia kwamba tunajiuzulu siasa kutokana na changamoto hizi. Tumeamua kupambana na kurudisha hadhi na heshima ya Chama chetu. Hatuwezi kubwaga manyanga. Tunataka kuitoa CCM madarakani kutokana na ulaghai na ujanja-ujanja wa miaka 50. Lakini hatuwezi kuitoa CCM kwa mbinu za ulaghai na ujanja-ujanja. Tunakwenda kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na Watanzania. Tunao wajibu wa kujiongoza vizuri ili tuwaonyeshe Watanzania kwamba tuna uwezo wa kuwaongoza vizuri.
WITO WETU
- Tunamshauri Mwenyekiti wetu, ndg. James Mbatia, aitishe vikao vya kikatiba ili tuweze kujadiliana kuhusu hatima ya chama chetu.
- Tunashauri ndg. Mbatia asiwemsemaji wa CHADEMA wakati anakiacha chama chake (NCCR-Mageuzi) kinadhoofika. Kwa mfano, Dr. Slaa alipoishambulia Chadema hakuna kiongozi wa Chadema aliyemjibu isipokuwa Mbatia ndiye aliyeamua kujiingiza kwenye ugomvi ndani ya Chadema.
- Tutachangishana ili tusafiri kwenye majimbo na kata za wagombea wetu na kuwasaidia kwenye kampeni ili wasibaki wapweke kama yatima.
- Tunasisitiza kwamba upinzani wa kweli nchini hauwezi kujengwa kwa njia za hila, kwa kukiuka taratibu za kidemokrasia tulizojiwekea wenyewe, kwa kukiuka misingi muhimu kama uadilifu, kwa kuweka mbele tamaa na maslahi binafsi kuliko taifa, kwa kutegemea propaganda. Tukifanya hivi, wananchi watashindwa kututoufautisha na CCM na wataamua kuchagua zimwi walijualo. Hatari hii tunaiona wazi kabisa.
……………………………
Leticia Ghati Mossore
Makamu Mwenyekiti (Bara)
NCCR-Mageuzi
17.09.2015
Mosena Nyambabe
Katibu Mkuu, NCCR Mageuzi