Moshi. Vijana 50 wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, 
wanadaiwa kufanya fujo kwenye mkutano wa hadhara wa mgombea wa ubunge wa
 CCM katika Jimbo la Moshi Mjini, Davis Mosha na kusababisha polisi 
wawatawanye kwa mabomu ya machozi.
Kamanda wa polisi 
mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea juzi 
katika eneo la Rau Madukani, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema
 mgombea wa CCM akiwa anatarajia kuzungumza na wanachi katika eneo hilo,
 kulitokea kundi la vijana wanaokadiriwa kufikia 50 wakiwa na silaha za 
jadi, marungu, mawe na fimbo na kuanza kuwashambulia watu waliokuwa 
katika mkutano wa mgombea huyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti 
wa Chadema katika Manispaa ya Moshi, Jafari Michael ambaye pia ni 
mgombea ubunge, alikanusha vijana wa Chadema kufanya vurugu hizo, bali 
alidai zilifanywa na vijana ambao hawajulikani wana itikadi ya vyama 
gani.
Michael alivilaumu vyombo vya dola kuwa vinawapendelea CCM kiasi cha kila jambo likifanyika huwatuhumu vijana wa Chadema.
"Hata
 tukipeleka malalamiko polisi hawatusikilizi na hata kama vurugu 
zikifanywa na wafuasi wa CCM wanasema ni Chadema, wanatuonea sana hawa 
jamaa," alilalamika Michael.
Alisema vijana waliokamatwa mtu hawezi kuwatuhumu moja kwa moja kuwa ni wa Chadema, kwa kuwa hawajulikani itikadi zao.
Kamanda
 Ngonyaji alidai kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baada ya wafuasi wa CCM 
kudaiwa kushusha bendera za Chadema zilizokuwa zimesimikwa uwanjani 
hapo.
Alisema vurugu hizo zilisababisha majeruhi wawili
 aliowataja kuwa Wilson Fabian (23) aliyepigwa jiwe kwenye paji la uso 
pamoja na mkono wa kulia, mwingine hakufahamika jina mara moja na wote 
walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.
Ngonyani alidai kuwa vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa magari yaliyokuwapo uwanjani hapo baada ya kuvunjwa vioo.
Alisema watu kumi na moja wanashikiliwa kwa mahojiano kutokana na vurugu hizo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
 


 
 
 
 
 
 
