Rais Jakaya Kikwete amesema watu wanaopanga 
kubaki katika vituo vya kupigia kura baada ya kumaliza zoezi hilo kwa 
lengo la kulinda kura kunaashiria uvunjaji amani, hivyo serikali 
imejipanga kupambana na hali hiyo siku ya uchaguzi.
Rais amesisitiza kwamba wanaopaswa kulinda kura ni mawakala pekee na si wafuasi wa mgombea ama vyama.
Akizungumza
 leo katika sherehe za Kilele cha Mwenge wa Uhuru zilizofanyika  Uwanja 
wa Jamhuri mjini Dodoma, kiongozi huyo anayemalizia muda wake madarakani
 amesema viongozi wanaowaagiza wafuasi wao kulinda kura wana nia mbaya 
dhidi ya amani ya nchi.
"Mnatakiwa 
muondoke kwenye vituo baada ya kupiga kura".kura utazilindaje? 
Mawakala ndio pekee wanaoweza kulinda. Mkikaidi hilo, hatutawavulimia. 
Serikali imejipanga kupambana na wale wote watakaokaidi agizo la Tume ya
 Uchaguzi (NEC),"amesisitiza Rais Jakaya Kikwete.
Katika
 shehere hizo za mwenge zinazoendana sambamba na maadhimisho ya siku ya 
kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Kikwete amewataka 
Watanzania kuchagua watu waadilifu ambao dhamira ya kupambana na rushwa 
kwa vitendo.
"Tumchague mtu ambaye 
hana ukabila, udini na ubaguzi wa rangi tumchague kiongozi 
atakayetetea maslahi ya makabila yote 126," amesema rais huku 
akimnukuu Mwalimu Nyerere aliyefariki miaka 16 iliyopita.
Sherehe
 hiyo imehudhuriwa pia na Spika wa Bunge anayemaliza muda wake, Anne 
Makinda, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa ngazi tofauti serikali na
 kupambwa na nyimbo za makabila na wanafunzi wa shule mbalimbali mjini 
Dodoma.
 


 
 
 
 
 
 
 
 
 
